Ni muhimu kukumbuka kuwa mara zote kila jambo huwa na chanzo chake. Neno #ElimikaWikiendi lilikuja mnamo mapema mwaka 2016, baada ya kudadavuliwa kutoka neno #ElimikaWeekend kupitia mtandao wa kijamii wa 'twitter'. Lengo kuu la kuanzishwa kwa neno hili #ElimikaWeekend chini ya mwanzilishi Paschal Masalu (akiwa Mwanafunzi wa Chuo Cha Usimamizi wa Fedha-IFM) lilikuwa ni kuwaleta pamoja watu wote wenye kuielewa lugha ya Kiswahili ili wazungumze pamoja kwa mlengo wa Kuikuza lugha mtandaoni, kuelimishana kwa kupitia lugha zawa ya Kiswahili pamoja na kuburudika. Baada ya kuonekana kuwa mwitikio wa watu ulianza kuwa mkubwa, watumiaji wa neno hilo #ElimikaWeekend wakashauri kuwepo kwa mabadiliko ya neno hilo ili lilete ukamilifu wa lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, #ElimikaWeekend ikabadilika na kuanza kuitwa #ElimikaWikiendi.

Neno #ElimikaWikiendi liliingia kwa kishindo kikuu mtandaoni na kuanza kutumiwa na wadau wengi wa Kiswahili hasa toka Tanzania na nchi jirani ya Kenya. Matumizi haya yalipelekea watu kuwa na uhitaji wa mada kamili ambayo ingeweza kujadiiwa ndani ya siku maalum. Kutokana na maombi hayo kuwa mengi, ikabidi utaratibu wa uendeshwaji wa #ElimikaWikiendi ubadilike, kutoka utumiaji huru wa neno hilo kwa kutuma jumbe yoyote, hadi kufikia kujadili mada mbalimbali zenye mlengo wa kuielimisha jamii.

#Elimikawikiendi imeendelea kufanya vema hata kufikia zaidi ya jumbe 2,500 (elfu mbili na miatano) kwa siku moja (yaani masaa ya kuendesha mada, ambayo mara nyingi huwa ni mawili hadi matatu). Kutokana na utumiaji huu mkubwa wa neno hili #ElimikaWikiendi, sasa wadau wa Kiswahili mtandaoni wamezidi kuongezeka na kuungana nasi kutuma jumbe zao za Kiswahili kila Jumamosi huku wakiambatanisha neno #ElimikaWikiendi.

Neno #ElimikaWkiendi limepewa maana nyingi za kimisamiati kama, Darasa, Daraja, Jamvi, Bakuli, Chumba cha Mahojiano n.k Hii ni kutokana tu na kupendwa na watu na kila mtu kutamani kukipa kipindi hiki jina litakalopendeza. Kutokana na hali hii, sisi #ElimikaWikiendi tumeamua kulitumika neno hili kama, "Zaidi ya Darasa", yaani pahala pa kupata elimu mchanganyiko, zaidi ya ile mtu awezayo kuipata darasani.

Hujachelewa bado, karibu ujumuike nasi kila ifikapo Jumamosi kupitia 'Twitter'. Andika tu neno #ElimikaWikiendi, nasi tutauona ujumbe wako na kuurusha kwa wadau wengine wa Kiswahili mtandaoni. 
Kiswahili kukua na kuzungumzwa na watu wengi mtandaoni ni jambo linalowezekana. Karibu, na tuwe pamoja. 

0 comments:

Post a Comment

Kutoka Twitter

Zilizo Maarufu

Tangaza Nasi

Tangaza Nasi

Tuachie Ujumbe