Wednesday 29 June 2016


Baada ya ukoloni kuisha afrika, jamii zetu zilianza kujitegemea kwa kila kitu; shughuli za kibiashara, siasa na kijamii (tamaduni, mila na desturi). Kila jamii ilikua na njia zake za kulea watoto na kwa asilimia kubwa zilikua zikilingana. Wazee walilea watoto wao na kuwarithisha malezi ambayo watoto waliweza kuwalea watoto wao sawa na walivyolelewa. 

Ni hadithi tulizo pata kutoka kwa wazazi wetu na bibi na babu zetu. Wanaume ndio walikua na sauti katika jamii, katika familia baba ndiye aliyekua na sauti na maamuzi juu ya familia, mlezi mkuu alikua ni mama kwani muda mwingi alikua na watoto, mara nyingi ushauri na tabia za watoto alikua akijua mama. Watoto hawakua na uwezo wa kutoa ushauri katika familia, ni mama na baba ndio wenye kauli na ushauri. Watoto walikua wakirithishwa malezi, tamaduni, mila na desturi kwa vitendo na maneno. Jinsi ya kuishi na watu, heshima na unyenyekevu kwa wakubwa na rika zao. 
Waazazi walikua wakiwafundisha shughuli za kufanya kwa vitendo na ukaribu; kulima, kuwinda, kufuga, kupika kwa ustadi mkubwa sana. 
Mtoto/kijana hakuwa na nafasi kubwa ya kujiamulia katika maisha yake, kwani alichaguliwa mke/mume wa kuoa au kuolewa nae. Mtoto alikuwa akichaguliwa na wazazi wake nini cha kusoma, nini cha kufanya kwa manufaa ya maisha yake ya baadae. Maisha ya watoto kwa asilimia kubwa yalikua chini ya uangalizi wa wzazi.

Watoto walijifunza tabia kupitia maisha ya wazazi wao na jamii zilizowazunguka. Mtoto wa kiume alikuwa na nafasi kubwa ya kuonekana kwani ndiye aliye onekana kuwa na faida katika jamii, alipendelewa katika elimu na shuguli za kibiashara. 
Mtoto wa kike hakupewa nafasi ya kubwa ya mchango katika vitu vingi kwasababu hakuonekana ana haki ya kupewa kipaumbele, zaidi ya kuelekezwa shughuli za nyumbani kama mlezi na kukaa nyumbani halikadhalika na shughuli za kilimo. Hali hii ilimpelekea mtoto wa kike kupungua uwezo wa kujiamini katika jamii. Kipindi hiki kuona mtoto mwenye tabia mbaya ni ajabu sana (walikuwepo, ila ilikua ngumu kuwaona). Jirani alikuwa na uwezo wa kumuadhibu mtoto wa mwenzake akikosea. 

“mtoto wa mwenzako ni wako pia…!” 

Mzazi alikua akimkanya mtoto anapokosea, na kumwambia yapi ni mazuri na yapi ni mabaya kwa mtoto kufanya kuepuka aibu kwa familia, jamii na kwake pia. Fimbo na maneno (methali, nahau, hadithi na misemo) vilitumika kumuonya na kumfundisha mtoto. Ilikua ni jamii inayopenda kutumia hayo kuhakikisha watu wanatunza na kuheshimu tamaduni za jamii husika. 

“asiye funzwa na mamae hufunzwa na ulimwengu…! 

Asiye sikia la mkuu huvunjika guu…! 

Busara, hekima na heshima ndiyo ngao…!” 

Ukitaka kujua tabia na mwenendo wa mtoto, ukimuuliza mama au baba au ndugu, ndiyo atakayo kuelezea jirani bila kuwa na utofauti mkubwa. Ubinafsi ulikuwa wakiwango kidogo sana kwani watu walikua wakitegemeana. Mambo yakaanza kubadilika baada ya elimu kushika kasi katika jamii zetu, muingiliano wa watu wenye, tamaduni, mila na desturi tofauti na jamii zetu. Wale watoto waliopokea zile mila na desturi na tamaduni kutoka kwa wazazi na vikongwe wakaanza kuathirika na vitu vipya kutoka sehemu zingine za dunia. Utaona aina ya maisha unayoishi wewe na jamii yako hayafai, pale utakapo vutiwa na aina ya maisha wanayoishi jamii zingine kutoka sehemu tofauti. Wazazi wakaona umuhimu wa kupeleka watoto mashuleni (wa kiume na wakike) ili kupata elimu itakayo wasaidia wao na wazazi wao. Na kuwaacha wajiamulie nini wanataka kufanya katika maisha yao ya baadae. Mwanamke alionekana kutotendewa haki, na kuanza kupiganiwa haki zake katika jamii zilizo kithiri mfumo dume; mwanamke ana haki ya kupata elimu, kuongoza, kufanya kazi. Harakati zilishika kasi kama moto wa vifuu sasa wakataka kuwa sawa na wanaume (haki sawa kwa wote: mwanamke afanye kazi sawa na mwanaume), zingine zilisikika zikitaka kumkomboa mwanamke kutoka jikoni mpaka ofisini. Matokeo yake sasa wametuzalishia wanawake wenye ujuzi wa kufuga kucha na sio wajuzi wa jikoni tena.

 “ukicheka na nyani utavuna mabua” 

Nimejiuliza sana, kwanini hizi harakati hazikupigania kuonesha na kueneza elimu dhidi ya umuhimu wa kila mmoja kutambua majukumu yake na nafasi yake katika jamii? Kitu ambacho ndicho jamii zetu zilikua zina kosa. Sasa wazazi wamejikita katika kufanya kazi na mambo mengine kwa dhana ya kuhakikisha watoto wao wanapata maisha na elimu bora ili waje kuwasaidia na kujisaidia. Watoto wanajifunza tabia kwa kuangalia maisha ya jamii zenye tamaduni tofauti na tuliyo sisi. Tabia za wazazi zina utofauti mkubwa na tabia za watoto. Wazazi wanatumia maeneno kuwakanya watoto wao juu ya maisha ya sasa. 

“Shauri yako na maisha yako, mimi yangu tayari ninayo…! 

Hunikomoi mimi unayofanya unajikomoa mwenyewe na maisha yako..! 

Mbwa wewe, usirudi hapa na jeuri zako, kinyago wee..!” 

Jirani hana tena uwezo wa kumkanya wala kumuadhibu mtoto wa mwenzake anapokosea “mtoto wa mwenzio mkubwa mwenzio babu/bibi wee..!” 

Watoto/vijana wanatembea na wazee wakubwa rika la wazazi wao bila haya wala soni. Hali hii imekua ni kawaida sana. Jamii za sasa hivi ni kitu cha kushangaza kuona mtoto mwenye tabia nzuri, tabia mbaya zimekua na nguvu kubwa kushinda nzuri. Haishangazi tena kuona watoto/wazee kuwa na tabia mbaya. Wanayojua wazazi juu ya mwenendo na tabia za mtoto ni tofauti na anavyojua jirani, na inaweza kua tofauti kabisa na mtoto mwenyewe alivyo. Wazazi sio tena walimu wa watoto wao, majukumu ya malezi yamesahaulika, walezi wapo kwenye mitandao. 
Kwa sasa tunahubiri maadili kwa maeno pasi na vitendo Teknolojia imekua kwa kasi kiasi cha jamii moja inaweza kuathirika na tamaduni za jamii nyingne bila muingiliano wa kivitendo. 

“jasiri haachi asili…!”. 

Huu msemo umezidiwa nguvu na maisha ya sasa, Asimilia kubwa haiwazi tena kurudia asili yake. Tumekuwa na jamii inayotumia nguvu kubwa kuipa nguvu ile sauti ndani mwetu yenye kuchochea mambo hasi kuidhoofisha ile inayopenda ukweli na mwongozo chanya katika maisha. Kuna mengi mazuri huko kwenye teknolojia. Lakini tukaamua kuchukua yale mepesi na yasio na umuhimu wa muda mrefu au mfupi pia. Watu wamekua wakiishi maisha ya kujiangalia wao bila kujali athari za aina ya maisha waliyochagua katika jamii iliyo wazunguka.

 “sijali maneno ya watu, hayanipunguzii wala kuniongezea kitu…! Naishi nitakavyo mimi,sitaki kupangiwa..! Kila mtu anaishi atakavyo yeye, kwaio tusiingiliane…!” 

“Hehehe, eeeh MUNGU NAOMBA UTUTANGULIE” 

Hakuna tena anae tamani kuwa kioo kwa jamii. Hakuna anaetaka kuwa mfano bora kwa jamii inayomzunguka wala kwa kizazi chake kijacho. Je kinachofanyika ni sawa? Je, Ni kweli hii teknolojia na muingiliano wa kitamaduni na mila zetu na za wengine zimesababisha kuharibika kwetu? Au ni sisi tuliamua kuchukua yale ambayo hayafai kutoka kwao, au tulichukua yaliyo mazuri kutoka kwao na kushindwa kuyafanya kwetu, kwasababu ya kushindwa kujua tutayatumiaje katika jamii zetu? Na Je, turudi nyuma tuanze upya? Au turekebishe na kuboresha yaliyobaki? Au tuendelee tu, kwani kitu gani? 

Mtunzi. 

BARAKA HEMEDI JEREKO

 ALHAMDULILLAH

0 comments:

Post a Comment

Kutoka Twitter

Zilizo Maarufu

Tangaza Nasi

Tangaza Nasi

Tuachie Ujumbe