Mara kadhaa, wazazi au walezi huwataka watoto wao wajifunze lugha ya ziada au nyingi ili tu wawe wa tofauti au kuwafikiria hapo baadaye kwenye maswala ya ajira. Lakini leo nimekuletea sababu sita za msingi kwanini wewe kama mtu mzima unatakiwa ujifunze lugha au kama mzazi unatakiwa kuhakikisha mtoto wako anajifunza lugha nyingi kadiri iwezekanavyo;
1. Huongeza nguvu ya ubongo
Kujifunza lugha nyingi huongeza uwezo wa ubongo wako kufikiri maradufu. Ni njia nzuri ya kufanya ubongo wako uwe na afya na sharp muda wote. Tafiti zinaonesha kuwa, watu wanaofahamu lugha nyingi huwa vizuri katika kuchakata lugha na maswala mengine ya kiuchambuzi. Kuweza kubadilisha kutoka lugha moja hadi nyingine husababisha sehemu ya ubongo wako inayohusika na utatuzi wa mambo na mchujo wa taarifa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Pia, ubongo ambao upo active husaidia kupunguza hatari za kupata magonjwa ya nyuroni kama vile dimetia.
2. Lugha ni geti la kuingia na kufahamu tamaduni nyingine
Lugha ni moja kati ya njia nzuri zaidi ya kujifunza kuhusu utamaduni mpya. Ukifahamu lugha fulani, itakufanya moja kwa moja uwe na shauku ya kufahamu kuhusu utamaduni fulani kwasababu mara nyingi, kufasiri jambo fulani kutoka katika lugha nyingine ili lieleweke katika lugha lengwa hushindwa kubeba maudhui yote yaliyokusudiwa katika muktadha wa jambo husika.
3. Utakuwa na uwezo wa kuwasiliana katika lugha nyingine
Kujifunza lugha nyingine hukulazimisha kuboresha uwezo wako wa kusikiliza na kuelewa na pia kukusaidia kuangalia lugha yako ya awali katika upande wa pili. Pia kujifunza lugha ya pili husaidia uweze kupata michongo na watu wengi zaidi na itakufanya uwe sehemu ya jamii inayozungumza lugha hiyo.
4. Inafanya kusafiri kwako kuwe rahisi na kufurahia
Kama unataka kuwa mtu anayesafiri kwenda sehemu mbalimbali duniani, basi kujifunza lugha ni jambo muhimu. Kusafiri ni njia ya kufurahia uzuri wa dunia na kujifunza mambo mapya, na kufahamu lugha fulani huondoa kikwazo katika kufanya hayo. Uwapo ugenini, hautohofia kuzurura hapa na pal3 kwasababu hauwezi kuwasiliana kirahisi,kwasababu utaweza kuzungumza na wenyeji bila kutegemea msaada wa vitabu vya utafsiri, lakini cha muhimu zaidi utajua chakula gani cha kuagiza bila ulazima wa kunyooshea kidole kwenye picha :)
5. Inakufanya Kuwa Open-Minded na kuondoa utofauti wa kitamaduni
Sababu kubwa ya ubaguzi wa kitamaduni na rangi ni kukosa uelewa kuhusu watu mbalimbali na utofauti katika tamaduni zao. Kufahamu lugha hutoa fursa pana ya kujifunza kuhusu wahusika wa lugha hiyo na tamaduni zao lakini pia husaidia wewe kuheshimu tamaduni za wengine. Muhimu pia, husaidia kuleta mshikamano, uvumilivu wa utamaduni na uelwa hasa katika mambo yanayohitaji ushirikiano kati ya watu tofauti ili kuyafanikisha.
6. Itakufanya uwe raia bora wa kidunia (Global Citizen)
Kama bado hujashitukia dili, faida na fursa zote zinazikuja na kujifunza lugha nyingi zitakufanya uwe raia bora wa dunia, Utajisikia na miguvu kila sehemu uwapo.Yapo mambo mengi ambayo ningependa tuzidi kuyajadili kupitia jamvi la #ElimikaWikiendi, hivyo nakuomba tuzidi kuwa pamoja.
Mwandishi & Mtunzi,
Kennedy Daima Mmary
Thanks for Sharing
ReplyDeleteThanks
ReplyDelete