Habari ndugu msomaji na Mtanzania mwenye
uzalendo na Taifa lake na mwenye dhamira ya wazi kabisa kuona kila kitu
kinachomilikiwa na Tanzania kinaweza kupiga hatua na kusonga mbele zaidi
ikiwemo Michezo, Muziki, Elimu, Nidhamu, Usalama, Amani, Demokrasia, Miundombinu,
Lugha ya Taifa pamoja na mambo mengine mengi yanayopatikana kwenye Nchi yetu
tuipendayo ya Tanzania. Kwanza kabisa nianze na maneno ya Hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambae ametuasa
tusiwe wabinafsi katika masuala yahusuyo taifa. Suala la ubinafsi
amelipiga vita tangu alipoasisi taifa hili na kutuagiza tuondokane na ubinafsi
kama alivyoandika katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe.’ Kitabu hiki
kilichapishwa mwezi wa Juni ya mwaka wa 1962. Kwa maana hiyo,
alitupa fursa ya kuielimisha jamii bila uchoyo na husuda kupitia njia mbali
mbali ikiwemo Mikutano ya hadhara, Semina na Mikusanyiko ya Hadhara mbali mbali
ili kuielimisha jamii ya Kitanzania.
Njia nyingine raisi ambayo watu wengi
tunaweza kujivunia sasa hivi kuna mitandao mingi ya kijamii ikiwemo tovuti
mbali mbali Mfano; jaliluzaid.com , chahali.com , millardayo.com , teknokona.com na nyingine nyingi
ambazo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kuelimisha jamii na kuhabarisha pia
jamii kwa lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili maana kupitia kuhabarika jamii
inapata kufahamu fursa mbali mbali za kimaendeleo hapa nchini na nje pia ya
Nchi.
Kutokana na kuwepo njia
mbali mbali za kuelimisha na kuhabarisha jamii bila ubinafsi wowote lugha ya
Taifa la Tanzania nikimaanisha Kiswahili imekuwa ikichukua nafasi kubwa na
kuweza kupanuka kwa kasi zaidi ikiwa ni pamoja na ndani ya Nchi na Dunia nzima
kwa ujumla.
Katika eneo la lugha,
tunayo mambo mengi tunayoweza kujifunza kwa faida yetu binafsi, kwa taifa letu
na kwa ulimwengu mzima kwa jumla. Hapa yafaa nitoe ufafanuzi kidogo.
Ni muda kidogo umepita
liko jambo lililotokea huko Uingereza ambalo ni mfano wa kuigwa. Wabunge
wa Bunge la Uingereza ambao ni wapenzi wa lugha yao ya taifa hawakuridhishwa na
hadhi ya lugha yao inavyotumika kitaifa na kimataifa. Waliweza kuishauri
Serikali yao iimarishe ufundishaji wa lugha ya Kiingereza katika shule
zote na hasa vyuo vya lugha. Pia waliishauri serikali kufundisha
Kiingereza kwa umakini mkubwa katika shule na vyuo. Pia walishauri kuwa shule
na vyuo vya lugha viongezewe fedha katika bajeti kila mwaka ili kupatiwa
fedha mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2011/2012. Pamoja na kutilia mkazo mafunzo
ya lugha yao, walisisitiza pia lugha za kigeni zisomeshwe kwa watu wa kada
mbalimbali hasa wanadiplomasia.
Kamati ya Mambo ya Nje
ya Bunge ilishauri kuwa kupandishwa vyeo kwa maofisa kutokane na ujuzi na
weledi wa Kiingereza pamoja na lugha moja ya kimataifa. Ambapo Serikali
ya Uingereza ilikubali bajeti kwa mafunzo ya lugha iongezeke kutoka $ 3 milioni
kwa mwaka 2011/12 hadi $ 3.9 milioni kwa mwaka 2013/14. Vilevile idadi ya
wanafunzi kwa mwaka iliongezwa na kuwa 1,000.
Hapa naomba tuzitambue
Lugha kubwa katika Dunia nzima kama lugha ya Mandarin, Kiarabu, Kihispania na
Kireno ni mioongoni mwa Lugha kubwa Duniani. Lugha ya Mandarin ni lugha
rasmi na lugha ya taifa la Wachina. Lugha ya Kihispania hutumika katika nchi za
Argentina, Chile, Uruguay, n.k. Kireno hutumika katika nchi
za Brazil, Cuba, Venezuela, n.k Kireno. Nchi za Argentina,
Chile, Uruguay, n.k. hutumia Kihispania. Lugha hizi
mbili hutumika katika nchi za Amerika ya Kusini. Lugha ya Kiarabu nayo
inatiliwa mkazo kama lugha muhimu na sababu kubwa ni za kiuchumi na kisiasa.
Katika bara la Afrika,
ziko lugha tofauti ambazo zinatufanya tusielewane kutokana na sababu za
kihistoria. Nchi za Afrika zinatumia lugha zenye asili ya kikoloni kama
Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kiingereza. Hizi ndizo lugha zinazotumika katika
vikao vya Umoja wa nchi za Afrika (AU).
Lugha ya Kiafrika
iliyokubaliwa kutumika katika shughuli za kikazi za AU ni Kiswahili.
Tanzania ilipewa jukumu la kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili kifikie hadhi
ya Kimataifa. Agizo hili lilitolewa mwaka 1988 huko Addis Ababa, Ethiopia. Na
mpaka sasa sisi tumefikia wapi tangu mwaka 1988 Tanzania ilipoteuliwa
katika kikao kilichofanyika huko Mauritus cha Mawaziri wa Umoja wa Nchi huru za
Afrika (OAU) na kuridhiwa na Wakuu nchi na serikali mwaka huo huo?
Kwa suala la ukuzaji wa
Kiswahili ndani ya nchi, mipango imekwama ya kukuza Kiswahili kutokana
na kutokuwepo kwa sera ya lugha iliyo wazi. Ni rai yangu kwa waziri mwenye
dhamana ya kusimamia lugha kuleta mawazo yakinifu yenye kuweza kutupeleka mbele
katika kukifanya Kiswahili kiwe ni lugha imara ya kitaifa na kimataifa.
Hapa nchini kwetu
kipo kituo cha kufundisha lugha za kigeni huko Zanzibar
linachojulikana kama Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI).
Hiki kituo kina
kila sababu ya kuitwa kituo cha lugha kwani kinafundisha lugha za kigeni
kama Kiarabu, Kiingereza , Kijerumani na Kifaransa katika ngazi ya
Diploma kikiwaandaa wataalamu wa ngazi ya kati. Pia kinafundisha Kiswahili kwa
wageni wanaokuja hapa nchini ama kufanya kazi au kujifunza Kiswahili ili
baadaye wakafundishe katika nchi zao.
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania itambue kuwapo kwa kituo hiki na kipatiwe fedha za
kutosha. Yanatakiwa maboresho ya hali ya juu ili kukiwezesha kituo hiki
kikidhi vigezo vya kimataifa; Kwa mfano wanatakiwa
wahadhiri wenye Shahada za Uzamili na Uzamivu katika lugha nilizotaja hapo juu
pamoja na vifaa vya kufundishia kama vitabu, video na baadae zisambazwe kupitia
Tovuti mbali mbali zikwemo jaliluzaid.com , chahali.com , millardayo.com , teknokona.com na zingine nyingi na
nzuri pia ili ulimwengu mzima upate kutambua ni kipi kinachoendelea
katika kituo hiki cha TAKILUKI na vilevile Maabara kisasa za
lugha kwa ajili ya kufundishia fonetiki, fonolojia na sintaksia ni kitu cha
muhimu sana.
Kutokana na kufanya haya
yote Kituo hiki kitawavutia wanafunzi wengi kutoka nje na Taifa
litapata fursa nzuri ya kujiongezea kipato pamoja na kuwaandaa Watanzania
kujipatia ajira nchi za nje na mwisho wa siku kuondoa huu wimbo wa Kila siku wa
kwamba hakuna ajira Tanzania.
Ahsante Kwa Kuisoma
Makala yangu hii Kama Utakuwa na Ushauri, Maoni nimeweka mawasiliano yangu hapo
mwanzo wa Makala Hii.
Mwandishi: Jalilu Zaid
Mwandaaji: Jalilu Zaid
0 comments:
Post a Comment