Wednesday 29 June 2016

Imeandaliwa na:  Jalilu Zaidi;

                      Barua Pepe: jaliluzaid@gmail.com 
                      WhatsApp: +255656587011.

Habari ndugu msomaji na Mtanzania mwenye uzalendo na Taifa lake na mwenye dhamira ya wazi kabisa kuona kila kitu kinachomilikiwa na Tanzania kinaweza kupiga hatua na kusonga mbele zaidi ikiwemo Michezo, Muziki, Elimu, Nidhamu, Usalama, Amani, Demokrasia, Miundombinu, Lugha ya Taifa pamoja na mambo mengine mengi yanayopatikana kwenye Nchi yetu tuipendayo ya Tanzania. Kwanza kabisa nianze na maneno ya   Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere ambae  ametuasa tusiwe wabinafsi katika masuala yahusuyo taifa.   Suala la ubinafsi amelipiga vita tangu alipoasisi taifa hili na kutuagiza tuondokane na ubinafsi kama alivyoandika katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe.’ Kitabu hiki kilichapishwa mwezi wa  Juni ya mwaka wa  1962. Kwa maana hiyo, alitupa fursa ya kuielimisha jamii bila uchoyo na husuda kupitia njia mbali mbali ikiwemo Mikutano ya hadhara, Semina na Mikusanyiko ya Hadhara mbali mbali ili kuielimisha jamii ya Kitanzania. 
Njia nyingine raisi ambayo watu wengi tunaweza kujivunia sasa hivi kuna mitandao mingi ya kijamii ikiwemo tovuti mbali mbali Mfano;  jaliluzaid.com , chahali.com , millardayo.com , teknokona.com na nyingine nyingi  ambazo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kuelimisha jamii na kuhabarisha pia jamii kwa lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili maana kupitia kuhabarika jamii inapata kufahamu fursa mbali mbali za kimaendeleo hapa nchini na nje pia ya Nchi.


Kutokana na kuwepo njia mbali mbali za kuelimisha na kuhabarisha jamii bila ubinafsi wowote lugha ya Taifa la Tanzania nikimaanisha Kiswahili imekuwa ikichukua nafasi kubwa na kuweza kupanuka kwa kasi zaidi ikiwa ni pamoja na ndani ya Nchi na Dunia nzima kwa ujumla.
Katika eneo la lugha, tunayo mambo mengi tunayoweza kujifunza kwa faida yetu binafsi, kwa taifa letu na kwa ulimwengu mzima kwa jumla. Hapa yafaa nitoe ufafanuzi kidogo.  

Ni muda kidogo umepita  liko jambo lililotokea huko Uingereza ambalo ni mfano wa kuigwa. Wabunge wa Bunge la Uingereza ambao ni wapenzi wa lugha yao ya taifa hawakuridhishwa na hadhi ya lugha yao inavyotumika kitaifa na kimataifa. Waliweza kuishauri  Serikali yao iimarishe ufundishaji wa lugha ya Kiingereza katika shule zote na hasa  vyuo vya lugha.  Pia waliishauri serikali kufundisha Kiingereza kwa umakini mkubwa katika shule na vyuo. Pia walishauri kuwa shule na vyuo vya lugha viongezewe fedha katika bajeti kila mwaka ili  kupatiwa fedha mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2011/2012. Pamoja na kutilia mkazo mafunzo ya lugha yao, walisisitiza pia lugha za kigeni zisomeshwe kwa watu wa kada mbalimbali hasa  wanadiplomasia.

Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge ilishauri kuwa kupandishwa vyeo kwa maofisa kutokane na ujuzi na weledi wa Kiingereza pamoja na lugha moja ya kimataifa.  Ambapo Serikali ya Uingereza ilikubali bajeti kwa mafunzo ya lugha iongezeke kutoka $ 3 milioni kwa mwaka 2011/12 hadi $ 3.9 milioni kwa mwaka 2013/14. Vilevile idadi ya wanafunzi kwa mwaka iliongezwa na kuwa 1,000.

Hapa naomba tuzitambue Lugha kubwa katika Dunia nzima kama lugha ya Mandarin, Kiarabu, Kihispania na Kireno ni mioongoni mwa Lugha kubwa Duniani.  Lugha ya Mandarin ni lugha rasmi na lugha ya taifa la Wachina. Lugha ya Kihispania hutumika katika nchi za Argentina, Chile, Uruguay,   n.k.  Kireno hutumika katika nchi za Brazil, Cuba, Venezuela, n.k   Kireno.  Nchi za  Argentina, Chile, Uruguay, n.k.  hutumia   Kihispania.  Lugha hizi mbili hutumika katika nchi za Amerika ya Kusini. Lugha ya Kiarabu nayo inatiliwa mkazo kama lugha muhimu na sababu kubwa ni za kiuchumi na kisiasa.

Katika bara la Afrika, ziko lugha tofauti ambazo zinatufanya tusielewane kutokana na sababu za kihistoria. Nchi za Afrika zinatumia lugha zenye asili ya kikoloni kama Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kiingereza. Hizi ndizo lugha zinazotumika katika vikao vya Umoja wa nchi za Afrika (AU).
Lugha ya Kiafrika iliyokubaliwa kutumika katika shughuli za kikazi za AU ni Kiswahili.  Tanzania ilipewa jukumu la kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili kifikie hadhi ya Kimataifa. Agizo hili lilitolewa mwaka 1988 huko Addis Ababa, Ethiopia. Na mpaka sasa sisi tumefikia wapi tangu mwaka 1988  Tanzania ilipoteuliwa katika kikao kilichofanyika huko Mauritus cha Mawaziri wa Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) na kuridhiwa na Wakuu nchi na serikali mwaka huo huo?  
Kwa suala la ukuzaji wa Kiswahili ndani ya nchi, mipango   imekwama ya kukuza Kiswahili kutokana na kutokuwepo kwa sera ya lugha iliyo wazi. Ni rai yangu kwa waziri mwenye dhamana ya kusimamia lugha kuleta mawazo yakinifu yenye kuweza kutupeleka mbele katika kukifanya Kiswahili kiwe ni lugha imara ya kitaifa na kimataifa.

Hapa nchini kwetu  kipo kituo cha kufundisha lugha za kigeni  huko Zanzibar linachojulikana kama Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI).
Hiki kituo  kina kila sababu ya kuitwa kituo cha lugha kwani kinafundisha  lugha za kigeni kama Kiarabu, Kiingereza , Kijerumani na Kifaransa katika ngazi ya Diploma kikiwaandaa wataalamu wa ngazi ya kati. Pia kinafundisha Kiswahili kwa wageni wanaokuja hapa nchini ama kufanya kazi au kujifunza Kiswahili ili baadaye wakafundishe katika nchi zao.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itambue kuwapo kwa kituo hiki na kipatiwe fedha za kutosha. Yanatakiwa  maboresho ya hali ya juu ili kukiwezesha kituo hiki kikidhi vigezo vya kimataifa; Kwa mfano wanatakiwa wahadhiri wenye Shahada za Uzamili na Uzamivu katika lugha nilizotaja hapo juu pamoja na vifaa vya kufundishia kama vitabu, video na baadae zisambazwe kupitia Tovuti mbali mbali zikwemo   jaliluzaid.com , chahali.com , millardayo.com , teknokona.com na zingine nyingi na nzuri pia ili ulimwengu mzima upate kutambua ni kipi kinachoendelea  katika kituo hiki cha TAKILUKI   na vilevile Maabara kisasa za lugha kwa ajili ya kufundishia fonetiki, fonolojia na sintaksia ni kitu cha muhimu sana.

Kutokana na kufanya haya yote  Kituo hiki kitawavutia wanafunzi wengi kutoka nje na  Taifa litapata fursa nzuri ya kujiongezea kipato pamoja na kuwaandaa Watanzania kujipatia ajira nchi za nje na mwisho wa siku kuondoa huu wimbo wa Kila siku wa kwamba hakuna ajira Tanzania.

Ahsante Kwa Kuisoma Makala yangu hii Kama Utakuwa na Ushauri, Maoni nimeweka mawasiliano yangu hapo mwanzo wa Makala Hii.

Mwandishi: Jalilu Zaid

Mwandaaji: Jalilu Zaid

0 comments:

Post a Comment

Kutoka Twitter

Zilizo Maarufu

Tangaza Nasi

Tangaza Nasi

Tuachie Ujumbe